Home Biashara Bei ya petroli kusalia vile, ile ya dizeli na mafuta taa yapungua...

Bei ya petroli kusalia vile, ile ya dizeli na mafuta taa yapungua kwa shilingi 2

0

Bei ya mafuta ya dizeli na mafuta taa imepunguzwa kwa shilingi mbili katika kipindi cha mwezi mmoja ujao.

Hii ni nafuu kiasi kwa Wakenya ambao wamelazimika kugharimika zaidi wakati wakinunua bidhaa za mafuta nchini kufuatia kuongezeka kwa bei za mafuta mwezi hadi mwezi.

Hata hivyo, Mamlaka ya Kudhibiti Bei za Mafuta nchini, EPRA inasema bei ya mafuta ya petroli itasalia vile.

Katika mapitio yake ya mwezi uliopita, EPRA iliongeza bei ya petroli kwa shilingi 5 na senti 72 kwa lita moja.

Kutokana na mapitio hayo, Wakenya katika kaunti ya Nairobi wamekuwa wakinunua lita moja ya petroli kwa shilingi 217 na senti 36, bei ambayo itaendelea kutumika katika kipindi cha mwezi mmoja ujao.

EPRA inasema imeamua kutoa ruzuku kwa bidhaa za mafuta katika kipindi cha mwezi Novemba hadi Disemba kutokana na gharama ya juu ya uagizaji wa bidhaa hiyo, lengo likiwa kuwakinga watumiaji dhidi ya kuongezeka kwa bei za mafuta nchini.

Inaongeza kuwa Wizara ya Fedha imetambua fedha zitakazotumiwa kuzifidia kampuni za mafuta.

 

Website | + posts