Serikali imetangaza kupunguza bei ya mbolea kutoka shilingi 3,500 hadi 2,500 kwa kila gunia la kilo 50.
Rais William Ruto ametangaza bei hiyo leo Jumatano katika Ikulu ya Nairobi akisema kuwa awamu ya pili ya usambazaji wa mbolea ilianza kutekelezwa Agosti mosi kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa chakula nchini.
Rais ameongeza kuwa serikali inaangazia kuzalisha magunia milioni 60 ya chakula kila mwaka kutokana na mpango wa serikali wa kusambaza mbolea ya bei nafuu.
Mwaka huu, serikali ina malengo ya kuzalisha magunia milioni 44 ya chakula, hili likiwa ongezeko la magunia milioni 12 ikilinganishwa na kiwango kilichovunwa mwaka uliopita.
Rais amewahimiza wakulima kote nchini kutumia mvua za vuli kupanda chakula kwa wingi.
Tayari Waziri wa Kilimo Mithika Linturi ameelezea matumaini kuwa wakulima kote nchini watapata mavuno mengi kufuatia usambazaji uliofanikiwa wa mbolea ya bei nafuu uliofanywa na serikali.
Ili kuongeza uzalishaji, Linturi ameiagiza Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao, NCPB kufungua vituo vipya vya kuuzia mbolea hiyo karibu na raia na kuwaajiri vibarua kusimamia vituo hivyo.
Hii ni kutokana na mashaka kwamba baadhi ya wakulima walishindwa kupata mbolea ya bei nafuu kutokana na gharama za juu za usafiri.
Linturi amesema vibarua hao watakuwa kiungo muhimu katika usambazaji wa mbolea ya bei nafuu kabla ya kuanza kwa msimu mfupi wa mvua.
Waziri aliyasema hayo alipofika mbele ya Kamati ya uwekezaji ya Bunge la Taifa inayoongozwa na mbunge wa Navakholo Emmanuel Wangwe.