Mwanariadha Bedan Karoki mwenye makao yake nchini Japan , amethibitisha kushiriki makala ya tatu ya mbio za Nairobi City Marathon Jumapili hii Septemba 8.
Karoki, ambaye alishinda nishani ya fedha ya katika mbio za dunia za nusu marathon mwaka 2016 mjini Cardiff, atakuwa akishiriki marathon kwa mara ya kwanza humu nchini.
Mwanariadha huyo aliye na umri wa miaka 34 pia alimaliza wa tatu lkatika mbio za London Marathon mwaka 2017, na anapigiwa upato kuwahemesha wanariadha wengine wa kutoka humu nchini na kimataifa siku ya Jumapili.
Mbio za marathon zimewavutia zaidi ya washiriki 1,000 watakaoshindania donge nono la shilingi milioni 3.5 kwa washindi ,2.2 kwa watakaomaliza nafasi za pili na milioni 1.5 kwa wale watakaotwaa nafasi za tatu.
Vitengo vingine vya mashindano ya Jumapili ni nusu marathon,kilomita 10 na kilomita 6.
Mbio za marathon zitaanza saa kumi na mbili na dakika 45 ,zikifuatwa na nusu marathon saa moja unusu na kilomita 10 saa tatu asubuhi.
Shindano hilo lililoasisiwa mwaka 2022 limeidhinishwa na chama cha kimataifa cha mbio za marathon na mashindano ya barabarani (AIMS).