Home Habari Kuu Bastola yapatikana Meru, polisi wamsaka mshukiwa

Bastola yapatikana Meru, polisi wamsaka mshukiwa

0

Polisi mjini Meru wanamsaka mwanamke mmoja anayeshukiwa kumiliki bastola kinyume cha sheria. 

Mwanamke huyo jana Jumapili usiku aliwakwepa wazee wa nyumba kumi katika eneo la Kabachi waliokuwa wakimsaka. Hii ni baada ya mshukiwa kudondosha mfuko wa manunuzi uliokuwa na bastola hiyo.

“Kawira Kanyaru alikuwa akitafutwa na wazee wakiongozwa na naibu chifu wa eneo hilo baada ya kupata habari kuwa huenda alifahamu aliko mshukiwa wa mauaji ambaye ametoweka,” imesema DCI katika taarifa.

Kabla ya kupatikana kwa bastola hiyo aina ya Retay Falcon, polisi waliamini ilikuwa mikononi mwa mshukiwa wa mauaji kwa jina Robert Meeme.

Meeme pamoja na babake Kawira, William Kanyaru na mshukiwa mwingine aitwaye  Japhet Johana ni washukiwa wa kesi ya mauaji yaliyotokea Februari 17, 2024 yanayohusiana na mzozo wa ardhi.

Bastola hiyo ilisalimishwa kwa kituo cha polisi cha Mutuati huku polisi wakianzisha msako mkali dhidi ya Kawira.