Home Habari Kuu Basi la Easy Coach lililobeba wanafunzi lahusika katika ajali Kisumu

Basi la Easy Coach lililobeba wanafunzi lahusika katika ajali Kisumu

0

Basi la kampuni ya Easy Coach limeripotiwa kuanguka katika mzunguko wa Mamboleo katika kaunti ya Kisumu jana Jumatatu usiku. 

Basi hilo lilikuwa limebeba wanafunzi wa shule ya upili ya wavulana ya Chavakali wakati likielekea jijini Nairobi ajali hiyo ilipotokea.

Inasemekana wanafunzi hao walikuwa wakielekea jijini Nairobi baada ya kufunga shule.

Chanzo cha ajali hiyo bado hakijathibitishwa.

Aidha taarifa za kina kuhusiana na hali ya wanafunzi hao bado hazijatolewa ingawa kumekuwa na ripoti kwamba mwanafunzi mmoja alifariki na wengine kujeruhiwa wakati wa ajali hiyo.

Kumekuwa na visa vingi vya ajali zinazowahusisha wanafunzi nchini katika siku za hivi karibuni.

Ajali ya hivi punde ilihusisha basi la Chuo Kikuu cha Moi lililokuwa limewabeba wanafunzi 65 likielekea Mombasa lilipopata ajali eneo la Kimende kwenye barabara ya Nakuru kuelekea Nairobi.

Kwa bahati nzuri, hakukuwa na majeruhi au vifo vilivyoripotiwa.

Wiki kadhaa zilizotangulia, kulikuwa na ajali iliyotokea eneo la Voi ikihusisha basi la Chuo Kikuu cha Kenyatta. Wanafunzi 11 walifariki wakati wa ajali hiyo na wengine kadhaa waliachwa wakiuguza majeraha.

Kabla ya kutokea kwa ajali hiyo, basi la shule ya upili ya Kapsabet pia lilihusika katika ajali iliyosababisha kifo cha mwanafunzi mmoja na mwalimu mmoja.