Home Habari Kuu Basi la abiria lashika moto kwenye barabara kuu ya Mombasa

Basi la abiria lashika moto kwenye barabara kuu ya Mombasa

0

Basi la abiria lililokuwa likielekea Nairobi kutoka Mombasa lilishika moto na kuteketea katika eneo la Kanga, kaunti ya Makueni kwenye barabara kuu ya kutoka Mombasa kuelekea Nairobi.

Ajali hiyo ya jana saa saba usiku iliripotiwa katika kituo cha polisi cha Mtito Andei.

Kamanda wa polisi wa eneo la mashariki Joseph Ole Napeiyan alithibitisha kisa hicho akielezea kwamba basi hilo lilikuwa na abiria 20 ambao wote waliokolewa pamoja na mizigo yao.

Napeiyan alisema maafisa wa polisi walifika eneo la tukio na kubainisha kwamba moto ulioteketeza basi hilo kabisa ulianzia kwenye gurudumu la upande wa nyuma.

Abiria walipatiwa gari jingine na kampuni inayomiliki basi lililochomeka ili kukamilisha safari yao hadi Nairobi.