Klabu ya Barcelona imempiga kalamu kocha wake mkuu Xavi Hernandez baada ya kuhudumu kwa kipindi cha miaka mitatu.
Aliyekuwa kocha wa Bayern Munich na Ujerumani Hansi Flick anatarajiwa kutwikwa jukumu.
Uamuzi huo wa kumpiga kalamu Xavi umetokea mwezi mmoja baada ya Rais wa Barcelona Joan Laporta kumsihi abaki klabuni humo alipotangaza kuwa angeondoka mwishoni mwa msimu wa 2023/24 .
Xavi mwenye umri wa miaka 44 ataiongoza Barcelona kwa mechi ya mwisho wa msimu Jumapili ijayo ugenini dhidi ya Sevilla kablaya kung’atuka.
“FC Barcelona inapenda kumshukuru Xavi kwa kazi yake kama kocha, na pia kwa kazi yake isiyo na kifani kama mchezaji na nahodha wa timu, na inamtakia mafanikio mema ya siku zijazo duniani.” ilisema taarifa ya Barcelona.
Xabi alijiunga na Barcelona Novemba 6, 2021 kuchukua nafasi ya Ronald Koeman na aliongoza timu hiyo kumaliza ya pili katika Ligi Kuu msimu wa 2021/22 .
Hata hivyo, Barcelona ilinyakua taji la LaLiga msimu wa 2022/23 pamoja na kombe la Super.
Xavi ataondoka Barcelona ikiwa kwenye nafasi ya pili nyuma Real Madrid waliotawazwa mabingwa .
Barca pia ilitumuliwa katikakipute cha Ligi ya Mabingwa ulaya msimu huu na katika awamu ya robo fainali na Paris Saint-Germain.
Mkataba wa Xavi ulitarajiwa kukamilika mwishoni mwa msimu ujao.