Wanahabari wamehimizwa wawe wakiangazia uanahabari wenye suluhu kama njia ya kutoa ushauri kuhusu suluhisho za matatizo mbali mbali yanayokumba jamii badala ya kuripoti tu.
Akizungumza mjini Meru wakati wa mafunzo kuhusu uanahabari wenye suluhu, mratibu wa eneo la kati na mashariki ya juu wa baraza la vyombo vya habari nchini Jackson Karanja alihimiza wanahabari kuwa sehemu ya usuluhishaji wa matatizo.
Alisema wanaweza kufanya hilo kupitia kuchapisha habari zinazolenga kusaidia jamii kusuluhisha matatizo mbali mbali wanayokumbana nayo.
Karanja alisema kwa miaka mingi, wanahabari wamekuwa wakiangazia matatizo kama jinai, athari za mabadiliko ya tabianchi, majanga, afya, elimu na mengine lakini wanakosa kuangazia suluhisho.
Kuhusu uhuru wa wanahabari, Karanja alisema ni muhimu kwa kila mmoja kuelewa kwamba uhuru huo umejikita kwenye katiba na hivyo wanahabari hawafai kushambuliwa au kushtuliwa wakitekeleza majukumu yao.
Aliwahimiza wajifahamishe kuhusu teknolojia inayozidi kukua akisema sasa uanahabari unaegemea sana teknolojia tofauti na miaka kadhaa iliyopita.
Mwenyekiti wa chama cha wanahabari wa Meru David Muchui na ripota Mugure Riungu walishukuru baraza la vyombo vya habari kwa mafunzo waliyopokea wakisema wamepata ujuzi muhimu.
Walilitaka bara hilo la vyombo vya habari MCK kuendelea kutoa mafunzo kama hayo kwa sababu uanahabari unabadilika kila wakati.