Home Kimataifa UNSC yakosa kuafikiana kuhusu Israel na Gaza

UNSC yakosa kuafikiana kuhusu Israel na Gaza

0

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, UNSC lilifanya mkutano wa dharura kuhusu vita vinavyoendelea kati ya Israel na kundi la Hamas lakini halikuafikiana kuhusu taarifa.

Kufikia sasa, watu zaidi ya 1,000 wameuawa tangu kundi la Kipalestina la Hamas ambalo linadhibiti ukanda wa Gaza kuanzisha mashambulizi katika miji mbalimbali ya Israel juzi Jumamosi.

Israel nayo ilijibu kwa kutangaza vita na kushambulia vikali eneo la Gaza lenye idadi kubwa ya watu ambapo wengi wamefariki.

Marekani, kwenye mkutano huo wa Baraza la Usalama ilitaka kundi la Hamas linyoshewe kidole cha lawama.

Akizungumza na wanahabari baada ya mkutano huo wa dharura, Robert Wood, mwanadiplomasia wa Marekani alisema nchi nyingi zimeshutumu mashambulizi ya Hamas lakini sio zote.

Alisema nchi ambazo hazijashtumu Hamas zinajulikana hata bila yeye kuzitaja akiashiria Urusi ambayo uhusiano wake na nchi za Magharibi umedorora tangu ivamie Ukraine.

Mkutano wa Baraza la Usalam la Umoja wa Mataifa ulichukua saa moja unusu ambapo baraza hilo lilipata taarifa kutoka kwa mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Mashariki ya Kati Tor Wennesland.

Wanadiplomasia wanasema wanachama wakiongozwa na Urusi wanatumai kwamba masuala ya kuangaziwa ni mengi na sio tu kulaumu Hamas.

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia alitaka vita hivyo visitishwe mara moja kisha pande husika ziingilie mazungumzo. Anahisi vita hivyo vimesababishwa na masuala ambayo hayakuwa yametatuliwa kwa muda mrefu.

Balozi wa Umoja wa Milki za Kiarabu – UAE katika Umoja wa Mataifa Lana Zaki Nusseibeh, alisema wanatarajia mikutano zaidi kuhusu mzozo wa Israel – Gaza akitumai kwamba kila mmoja anaelewa hali ni mbaya.

UAE ililainisha uhusiano wake na Israel mwaka 2020 kwenye mapatano ya kipekee.

Baraza hilo la Usalama lenye wanachama 15 huafikia makubaliano kupitia kupiga kura.

Wawakilishi wa Israel na Palestina katika baraza hilo hawakuhudhuria mkutano huo na balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa  Riyad Mansour kwa upande wake anataka wanadiplomasia hao waangazie kukomesha hali ya Israel kuingilia Gaza.

 

 

Website | + posts