Home Habari Kuu Baraza la Mawaziri: Kaunti 38 zimeathiriwa na mafuriko

Baraza la Mawaziri: Kaunti 38 zimeathiriwa na mafuriko

0

Jumla ya kaunti 38 zimeathiriwa na mafuriko yanayoshuhudiwa kutokana na mvua za El Nino zinazonyesha katika maeneo mbalimbali nchini. 

Watu 76 wamefariki huku familia 35,000 zikipoteza makazi.

Kaunti zilizopo Pwani na Kaskazini mwa nchi ndizo zilizoathirika zaidi na mafuriko hayo.

Aidha baadhi ya kaunti za eneo la katikati mwa nchi, magharibi na mashariki pia zimeathirika.

kaunti hizo ni pamoja na Mombasa, Mandera, Wajir na Makueni.

Akiwahutubia wanahabari kuhusiana na mkutano wa Baraza la Mawaziri ulioongozwa na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi leo Jumatatu, Msemaji wa Ikulu hiyo Hussein Mohamed alisema serikali kuu imeazimia kuongeza maradufu jitihada za kukabiliana na athari za mafuriko.

Kulingana naye, shilingi bilioni 7 zimetengwa na serikali kuu kushughulikia hali ya mambo katika kaunti zilizoathiriwa na mafuriko.

Serikali za kaunti zimetakiwa kutenga fedha kutoka kwa bajeti zao ili kushughulikia athari za mafuriko huku Mohamed akiashiria mgao wa shilingi bilioni 10 ulitolewa kwa serikali za kaunti wiki jana.

Mgao wa shilingi zingine bilioni 10 utatolewa kufikia mwishoni mwa wiki hii, yamkini kufikia siku ya Alhamisi.

 

 

Website | + posts