Home Taifa Bajeti kupunguzwa kwa shilingi bilioni 177, bilioni 169 kukopwa

Bajeti kupunguzwa kwa shilingi bilioni 177, bilioni 169 kukopwa

0
kra

Jumla ya shilingi bilioni 177 zitapunguzwa kwenye bajeti ili kukidhi sehemu ya nakisi ya jumla ya shilingi bilioni 346 iliyotokana na kukataliwa kwa Mswada wa Fedha 2024. 

Akihutubia taifa katika Ikulu ya Nairobi leo Ijumaa, Rais William Ruto amesema serikali itakopa shilingi zingine bilioni 169 ili kukidhi nakisi iliyosalia.

kra

Ruto amesema serikali imejikuna kichwa kuhusiana na namna ya kukabiliana na nakisi hiyo kabla ya kufikia uamuzi huo.

Alisema iliwazia kupunguza nakisi ya shilingi zote bilioni 346 kwenye bajeti lakini ikabainika kuwa hatua hiyo ingeathiri mno utekelezaji wa miradi mbalimbali ya serikali ikiwa ni pamoja na kuajiriwa kwa walimu wa JSS na mpango wa kutoa mbolea ya ruzuku kwa wakulima.

Aidha, Rais Ruto alisema kukopa jumla ya shilingi bilioni 346 kungekuwa na athari kubwa kwa taifa hili ikiwa ni pamoja na kuathiri kiwango cha ubadilishanaji wa fedha za kigeni.

Mswada wa Fedha 2024 ulikusudia kukusanya shilingi bilioni 346 kupitia utozaji kodi lakini ukapingwa vikali na Wakenya.

Kiini cha pingamizi hizo kilikuwa hoja kuwa ulikusudia kuwaongezea kodi nyingi wakati tayari wameeleemewa na mzigo wa maisha.

Maandamano ya kupinga mswada huo yamekuwa yakiendeshwa nchini na vijana wa Gen Z na kusababisha vifo vya watu kadhaa na kujeruhiwa kw mamia ya wengine.

Website | + posts