Mahakama ya Milimani jijini Nairobi leo Jumatano imetupilia mbali kesi iliyomkabili mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino na washtakiwa wenzake sita.
Uamuzi huo unafuatia ombi la Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga kutaka kesi dhidi yao kutupiliwa mbali.
“DPP baada ya kupitia mashtaka na uamuzi wa Jaji wa Mahakama Kuu ambaye alibatilisha kifungu cha 77(1) cha katiba kilichotumiwa kuwashtaki washtakiwa, aligundua kuwa kesi dhidi yao ni kinyume cha katiba,” Ingonga aliiambia mahakama kupitia kwa wakili James Gachoka.
Uamuzi wa kuwaondolea saba hao mashtaka ulitolewa na Jaji Lucas Onyina baada ya kuzingazia mawasilisho ya upande wa mashtaka.
“Nimezingatia mawasilisho, maombi yaliyotolewa na upande wa mashtaka yanatafakariwa na hivyo basi kesi hiyo kusitishwa,” alisema Jaji Onyina.
Babu alikamatwa wakati wa maandamano ya kitaifa dhidi ya serikali yaliyopangwa na muungano wa Azimio la Umoja kupinga gharama ya juu maisha.
Alishtakiwa pamoja na Calvina Okoth Otieno almaarufu Gaucho, Tom Ondongo Ong’udi, Michael Otieno Omondi, Pascal Ouma, Kevin Wambo na Willys Owino Baraka.
Mawakili wa upande wa washtakiwa wakiongozwa na Danstan Omari na Dancun Okatch waliambia mahakama kuwa kesi inayowakabili wateja wao ilichochewa kisiasa.
“DPP alifungua mashtaka dhidi ya washtakiwa akijua ni ya kisiasa, tunafurahi kwamba wametuma maombi ya kuondoa mashtaka,” alisema Okatch.