Home Kimataifa Baadhi ya wazee wa Njuri Ncheke wakubali kupatanisha Gavana na wawakilishi wadi

Baadhi ya wazee wa Njuri Ncheke wakubali kupatanisha Gavana na wawakilishi wadi

0
kra

Baadhi ya wanachama wa baraza la wazee wa jamii ya Ameru Njuri Ncheke wamekubali kufuata maagizo ya mahakama kuu ya Meru ya kupatanisha Gavana Kawira Mwangaza na wanachama wa bunge la kaunti ya Meru.

Maagizo hayo yalitolewa na jaji Linus Kassan wa mahakama hiyo kwenye kesi iliyowasilishwa na Mwangaza kutafuta kukomesha mjadala wa kumwondoa mamlakani.

kra

Awali baraza hilo la wazee likiongozwa na katibu mkuu wa kitaifa Josphat Murangiri, lilikataa kuhusika na jaribio la kumwondoa mamlakani Gavana Mwangaza kwa madai kwamba ni suala la kikatiba ilhali wazee hao hushughulikia masuala ya kijamii.

Wakizungumza katika maabadi ya Njuri Ncheke huko Ncheru kaunti ndogo ya Tigania Magharibi kaunti ya Meru baadhi ya wazee hao wakiongozwa na mwenyekiti wa tawi la Tigania la Njuri Ncheke Andriano Aruyaru, wazee hao walikana madai kwamba hawana uwezo wa kusuluhisha suala hilo.

Jaji wa mahakama kuu ya Meru Linus Poghon Kassan, alisimamisha jaribio la nne la kumwondoa mamlakani Gavana Mwangaza baada ya bunge kuarifiwa kuhusu ujio wa mjadala huo.

Alielekeza wazee hao kutatua suala hilo, kupatanisha Gavana na wawakilishi wadi na kufikisha ripoti mahakamani katika muda wa wiki tatu.

Kundi la wazee wa baraza hilo linaloongozwa na Aruyaru, limesema kwamba lina uwezo wa kutekeleza maagizo ya mahakama kuu ya Meru huku wakikashifu kundi lililokataa.

Kulingana na kundi hilo, Josphat Murangiri tayari amefurushwa kutoka kwa baraza la Njuri Ncheke hata kabla ya maagizo ya mahakama na kumhimiza alipe faini ili arejeshwe.

Murangiri amelaumiwa pia kwa kuwalisha kiapo baadhi ya wawakilishi wadi wa kaunti ya Meru katika maabadi ya Njuri Ncheke kinyume na mila za wazee hao.

Walilazimika kufanya matambiko ya kutakasa maabadi hayo huku wakialika Gavana Mwangaza na wawakilishi wadi kujiunga nao katika meza ya mashauriano ili kutatua zogo lao.

Gavana Kawira Mwangaza anakabiliwa na jaribio la tano la kumwondoa afisini baada ya mwasilishaji wa hoja ya awali kuwasilisha nyingine ya mjadala wa kumwondoa afisini.

Katika hoja hiyo, mwakilishi wasi mteule Ziporrah Kinya ambaye pia ni naibu kiongozi wa walio wengi bungeni anamlaumu Mwangaza kwa mwakosa matatu; matumizi mabaya ya fedha za umma, matumizi mabaya ya mamlaka na ukiukaji mkubwa wa maadili.

Website | + posts
Jeff Mwangi
+ posts