Home Habari Kuu Baadhi ya mifugo walioibwa warejeshwa Meru

Baadhi ya mifugo walioibwa warejeshwa Meru

0

Waziri wa usalama wa ndani Profesa Kithure Kindiki amepongeza maafisa wa usalama ambao walipambana na wezi wa mifugo na kurejesha baadhi ya mifugo walioibwa huko Meru.

Haya yanajiri wakati ambapo serikali ina wasiwasi kuhusu ongezeko la wizi wa mifugo katika eneo la Meru Kaskazini ambao unatekelezwa na wahalifu waliojihami katika muda wa mwezi mmoja uliopita.

Kindiki ambaye aliandaa mkutano na kamati ya usalama na ujasusi ya eneo la mashariki mwa nchi, kamati ya usalama ya kaunti ya Meru na kamati ya usalama ya kaunti ndogo ya Mutuati anasema usalama umeimarishwa katika eneo hilo.

Kulingana naye, kambi zaidi za maafisa wa kitengo cha kukabiliana na wizi wa mifugo na za kitengo cha GSU zimejengwa katika eneo hilo huku polisi wa akiba wapatao 140 wakianza mafunzo ya kikazi leo.

Waziri alisema kwamba mipango inaendelea ya kuhakikisha kwamba mifugo waliosalia wanarejeshwa.

Kindiki alisema ni lazima wanasiasa wakome kuingiza siasa kwenye oparesheni za kiusalama akisema kiongozi yeyote ambaye anachochea, kufadhili au kupanga wizi wa mifugo atakabiliwa vilivyo bila kuzingatia ushawishi wake kisiasa.

Makamanda wa vikosi vya kukabiliana na wizi wa mifugo, GSU na makundi mengine ya usalama katika eneo hilo pia walihudhuria mkutano huo wa usalama na waziri Kindiki.

Website | + posts