Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya juma lijalo, utaelekea mahakamani kwa lengo la kusimamisha utekelezwaji wa mswada wa fedha wa mwaka 2023.
Wakiongozwa na mbunge wa Rarieda Otiende Amollo na Gavana wa Siaya James Orengo, wabunge wa Azimio walisema kutangaza uhalali wa mswada huo ambao umeibua hisia mseto kutoka kwa Wakenya kuhusu mapendekezo ya ushuru yatakuwa makosa makubwa.
Wabunge hao wakiwemo John Mbadi (Mbunge mteule), Babu Owino (Embakasi Mashariki), Samuel Atandi (Alego – Usonga), Seneta Oburu Oginga (Siaya) na Enock Wambua (Kitui), walionya kutosherehekea kupitishwa kwa msaada huo, wakiongeza kuwa upinzani una njia mbadala wa kusimamisha kutekelezwa kwa mswada huo.
Waliyasema hayo katika kanisa la St. Sylvester eneo bunge la Rarieda wakati wa siku ya elimu kwa shule 21 zinazofadhiliwa na kanisa katoliki katika parokia ya Madiany.
Otiende Amollo alitangaza kuwa atafika mahakamani kesho Jumatatu kutafuta mwelekeo wa mahakama kuhusu uhalali wa mswada huo unaosubiri kutiwa saini kuwa sheria na Rais William Ruto.
Muungano huo siku ya Alhamisi ulitangaza kuwa utaandaa mkutano wa hadhara siku ya Jumanne, Juni 27 katika uwanja wa Kamukunji kuujadili mswada huo wa fedha na bajeti ya kitaifa.