Home Habari Kuu Azimio kuamua mwelekeo Jumanne baada ya Mswada wa Fedha kupitishwa bungeni

Azimio kuamua mwelekeo Jumanne baada ya Mswada wa Fedha kupitishwa bungeni

0
Martha Karua, aliyekuwa mgombea mwenza wa Azimio wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.
Martha Karua, aliyekuwa mgombea mwenza wa Azimio wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.

Muungano wa Azimio utaamua Jumanne ijayo, Juni 27, 2023 mwelekeo wa kuchukua baada ya jitihada zake za kupinga Mswada wa Fedha 2023 kuambulia patupu.

Mswada huo ulipitishwa katika bunge la Kitaifa jana Jumatano.

Kupitia kiongozi wa chama cha Narc K Martha Karua, muungano huo unasema utakata kauli ya mwelekeo wa kuchukua baada ya kushauriana na Wakenya.

“Tumeamua kuwaalika Wakenya katika uwanja wa Kamukunji Jumanne wiki ijayo, Juni 27, 2023 saa 4 asubuhi, ambapo hatua itakayofuata itaamuliwa,” alisema Karua wakati akiwahutubia wanahabari jijini Nairobi leo Alhamisi.

“Kila wakati ambapo kama watu tumekuja pamoja, tumepata suluhisho hata kwa matatizo yetu mabaya zaidi.”

Hata hivyo, alipobanwa na wanahabari kueleza ikiwa kuelekea mahakamani ni moja ya njia wanazowazia, Karua alidinda kubaini hilo akisema ni miongoni mwa mambo yatakayofafanuliwa wakati wa mkutano utakaofanyika Jumanne.

Muungano wa Azimio siku zilizopita umetumia maandamano kama njia ya kuishinikiza serikali kusikiliza vilio vyake, ila wakati huu, Waziri wa Usalama wa Taifa Kithure Kindiki ameonya kuwa yeyote atayethubutu kuvuruga amani ya nchi atakiona cha mtema kuni.

Karua kwa upande wake anasema kama upinzani, hawawezi wakatishwa na mtu yeyote kwani maandamano yamekubaliwa kikatiba.

Aidha kiongozi huyo alilalama kuwa kupitishwa kwa Mswada wa Fedha 2023 kutafanya maisha kuwa magumu hata zaidi na kuwapora Wakenya fedha chache walizokuwa nazo.

Hususan, alilamikia kuongezwa kwa ushuru wa asilimia 16 wa thamani ya ziada, VAT kwa mafuta kutoka asilimia 8 akisema hatua hiyo itafanya maisha kuwa magumu hata zaidi.

“Kufuatia ushuru mbalimbali uliopitishwa na bunge jana, lazima tujiandae kwamba hata fedha chache tulizokuwa tumesalia nazo zitatoweka,” alionya Karua.

Bunge la Kitaifa jana Jumatano lilipitisha Mswada wa Fedha 2023 baada ya siku nyingi za hali ya vuta ni kuvute.

Mswada huo ulipitishwa baada ya kusomwa kwa mara ya tatu.

Miongoni mwa mapendekezo tata yaliyopitishwa ni kuongezwa kwa ushuru huo wa asilimia 16 wa thamani ya ziada kwa mafuta kutoka asilimia 8.

Wabunge wapatao 184 waliunga mkono mswada huo huku 88 wakiupinga.

Ushuru wa ujenzi wa nyumba ulipitishwa baada ya kufanyiwa marekebisho na kupunguzwa hadi asilimia 1.5 ya mshahara kabla ya matozo.

Awali, ushuru huo ulipendekezwa kuwa asilimia 3.

Mswada huo sasa unasubiri tu kutiwa saini na rais kuwa sheria.

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here