Awamu ya pili ya maonyesho ya vifaa vinayotumiwa katika ujenzi nchini Uganda itaandaliwa mwezi huu kati ya tarehe 10 na 12 Agosti, 2023, katika uwanja wa UMA jijini Kampala.
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Miji nchini Uganda imetangaza kwamba inafadhili maonyesho hayo kwa ushirikiano na kampuni ya huduma za kibiashara ya India ETSIPL na Futurex.
Kampuni hizo mbili zinafahamika sana kwa maandalizi ya maonyesho ya kimataifa ya sekta ya ujenzi hasa barani Afrika, Asia, Uingereza, na Mashariki ya Kati.
Maonyesho hayo kwa jina “Uganda Buildcon International Expo” yataangazia usanifu mijengo, ujenzi, mashine zinazotumika, vifaa vya ujenzi, ubunifu, mapambo ya ndani na masuala mengine katika sekta nzima ya ujenzi.
Mipango ya serikali ya Uganda pamoja na sera zake katika sekta ya ujenzi pia itaangaziwa kwenye maonyesho hayo.
Kampuni za HISENSE na INGCO ndizo wafadhili wakuu wa maonyesho hayo kwa ushirikiano na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Miji, Wizara ya Biashara Ndogo Ndogo na za Kati, serikali ya India, muungano wa watengenezaji bidhaa nchini humo UMA na kongamano la masoroveya.
Maudhui ya awamu ya pili ya maonyesho ya ujenzi nchini Uganda ni “Ungana na tasnia ya ujenzi kujenga kesho bora”.