Home Kimataifa Austin azuru Ukraine kuihakikishia usaidizi wa Marekani

Austin azuru Ukraine kuihakikishia usaidizi wa Marekani

0
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin amefanya ziara ya kushtukiza mjini Kyiv, Ukraine ili kuihakikisha nchi hiyo kuwa Marekani itaendelea kutoa usaidizi wake dhidi ya uvamizi wa vikosi vya Urusi. 

Marekani imetoa mabilioni ya dola kama msaada wa usalama kwa Ukraine na mara kwa mara kuahidi kuisaidia Ukraine “kadiri ya muda ambavyo vita hivyo vitadumu.”

Lakini upinzani kutoka kwa wabunge wenye misimamo mikali wa chama cha Republican umeibua mashaka juu ya mustakabali wa msaada huo.

Austin “alisafiri kuelekea Ukraine leo kukutana na viongozi wa Ukraine na kusisitiza usaidizi wa Marekani kwa vita vya kujikomboa vya Ukraine,” ilisema Wizara ya Ulinzi wakati wa ziara hiyo ambayo awali haikutangazwa kutokana na mashaka ya usalama.

“Pia atasisitiza dhamira ya Marekani kuendelea kuipatia Ukraine msaada wa kiusalama ambao inauhitaji kujilinda dhidi ya uvamizi wa Urusi,” ilisema.

Ziara ya Austin mjini Kyiv ni ya pili tangu Urusi ilipoanzisha uvamizi kamili dhidi ya Ukraine Februari, 2022.

Marekani inasema ndio nchi ambayo imetoa kiwango kikubwa zaidi cha msaada wa kijeshi kwa Ukraine, na kupunguzwa kwa msaada wa Marekani kutakuwa pigo kubwa kwa Ukraine wakati ikijiandaa kwa msimu wa pili wa baridi wa vita hivyo.

Austin na Waziri wa Mambo ya Nje Antony Blinken walito wito kwa wabunge wakati wa kikao kilichoandaliwa mwezi Oktoba kuendelea kuisaidia Ukraine huku Austin akisema “bila usaidizi wetu, (Rais Vladimir) Putin atafanikiwa.”

AFP