Muungano wa vyama vya wafanyakazi, COTU bado uko imara na utaendelea kufanya kila uwezalo kutetea maslahi ya wafanyakazi kote nchini na duniani.
Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli anasema muungano huo unawakilisha wafanyakazi zaidi ya milioni nne na ni wa pili kwa ukubwa barani Afrika.
Kwa misingi hiyo, Atwoli anasema COTU itaendelea kuwawakilisha vilivyo wafanyakazi ndani na nje ya nchi hii.
“Tunaamini mno katika kanuni za majadiliano ya jamii, ushirikiano kati ya vyama vya wafanyakazi, waajiri na serikali, na utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani,” alisema Atwoli katika taarifa leo Jumatatu asubuhi.
“Tunatambua wajibu wetu kama muungano wa wafanyakazi unaowajibika ni kushiriki mazungumzo yenye tija na serikali, waajiri na wadau wengine wakuu ili kutetea haki na maslahi ya wafanyakazi.”
Atwoli aliyasema hayo kufuatia taarifa zilizoangaziwa katika gazeti moja la humu nchini zikiashiria kuwa vyama vya wafanyakazi nchini hususan muungano wa COTU vimekosa makali ya kutetea maslahi ya wafanyakazi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Awali, kiongozi wa upinzani Raila Odinga pia amemkosoa Atwoli kwa kuwatelekeza wafanyakazi wakati akishirikiana na utawala wa Kenya Kwanza kupigania maslahi ya kibinfasi, madai ambayo Atwoli ameyapuuzilia mbali.
Akiwa mfuasi sugu wa muungano wa Azimio kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, Atwoli ameonekana kubadili mwelekeo na ameapa kufanya kazi na serikali ya Rais William Ruto kupigania maslahi ya wafanyakazi nchini.
Na huku baadhi ya vyombo vya habari vikizidi kukosoa utendakazi wa vyama vya wafanyakazi nchini, Atwoli anatoa wito kwa Baraza la Vyombo vya Habari Nchini, MCK na Chama cha Wahariri Nchini kuwachukulia hatua wahariri waandamizi anaodai wamejitwika jukumu la kuyaharibia sifa mashirika na watu binafasi kupitia uandishi wa taarifa zinazopotosha.
“Msimamo wetu umejikita kwa ukweli kwamba Kenya inakabiliwa na changamoto kubwa za kiuchumi. Katika hali ngumu kama hizi, ni muhimu kwetu sisi sote kufanya kazi kuelekea kuhakikisha uchumi unakuwa thabiti, kulinda ajira na kubuni mazingira mwafaka ya ukuaji uchumi endelevu,” aliongeza Atwoli wakati akivitaka vyombo vya habari kutoa habari sahihi na zisizoegemea upande wowote kwa umma.