Katibu mkuu wa muungano wa vyama vya wafanyakazi nchini, COTU Francis Atwoli amemtaka mbunge wa Ikolomani Benard Shinali atupilie mbali mswada wake unaopendekeza Wakenya watozwe ushuru zaidi.
Akizungumza huko Khwisero katika kaunti ya Kakamega, Atwoli alisema kwamba wafanyakazi wa Kenya tayari wanatozwa kiwango cha juu cha ushuru na kuwaongezea kutawazidishia matatizo ya kiuchumi.
Shinali ametayarisha mswada ambao unapendekeza wafanyakazi watozwe ushuru wa asilimia moja na waajiri wawatolee asilimia moja nyingine pesa ambazo zitakwenda kwenye hazina ya bima ya ukosefu wa ajira.
Shinali alimotishwa na hali ilivyo nchini Afrika Kusini ambapo wafanyakazi wanatozwa asilimia moja ya mshahara na waajiri wanawatolea asilimia nyingine moja pesa ambazo huenda kwa hazina ya kusitiri wanaopoteza ajira.
Kando na kuanzisha hazina hiyo ya bima ya ukosefu wa ajira, mswada wa Shinali unapendekeza kubuniwa kwa mamlaka ambayo itakuwa ikisimamia bima hiyo.
Matamshi ya Atwoli yanajiri wakati ambapo gharama ya maisha imepanda kutokana na kuongezwa kwa ushuru wa kuongeza thamani kwa bidhaa na wakati wafanyakazi wameanza kutozwa asilimia 1.5 ya mshahara na waajiri wakiongeza asilimia 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba.