Home Kimataifa Askofu Anyolo atilia shaka kutokuwepo kwa upinzani nchini

Askofu Anyolo atilia shaka kutokuwepo kwa upinzani nchini

Anyolo aliyasema hayo kutokana na imani yake kwamba serikali ni lazima iwe na watu wa kuikosoa.

0
Askofu Mkuu Philip Anyolo
kra

Askofu mkuu wa dayosisi ya Nairobi ya kanisa katoliki Philip Anyolo ametilia shaka kutokuwepo kwa upande wa upinzani nchini ikikumbukwa kwamba Rais Ruto aliteua wanachama wa ODM kuwa mawaziri.

Akizungumza wakati wa ibada ya Jumapili katika kanisa la Mtakatifu Annah huko Kabete, kaunti ya Kiambu Anyolo alihimiza vyama vingine tanzu vya muungano wa Azimio la Umoja One Kenya kuhakikisha vinaunda upinzani thabiti.

kra

Anyolo aliyasema hayo kutokana na imani yake kwamba serikali ni lazima iwe na watu wa kuikosoa.

Wakati huo huo Askofu mkuu Anyolo aliwataka wabunge wasikilize na kutekeleza matakwa ya wakenya wakati wa kusaili mawaziri wateule kabla ya kuwaidhinisha.

Usaili wa wateule hao wa nyadhifa za uwaziri utaandaliwa katika majengo ya bunge kati ya Agosti Mosi na Agosti nne mwaka huu wa 2024.

Rais William Ruto aliteua wanachama wanne wa chama wa ODM kwenye baraza lake jipya la mawaziri hatua iliyowafanya wengi kuamini kwamba upinzani umeingia kwenye mapatano na serikali ya Kenya Kwanza.

Hata hivyo kiongozi wa upinzani Raila Odinga anasisitiza kwamba hakuna mkataba ulioafikiwa na kwamba wanachama hao wa ODM iwapo wataidhinishwa watafanya kazi kwa kuzingatia sera za chama cha ODM.