Home Habari Kuu Asilimia 80 ya maafisa wa polisi watakaoajiriwa watatoka NYS

Asilimia 80 ya maafisa wa polisi watakaoajiriwa watatoka NYS

Zoezi hilo la kuajiri polisi linatarajiwa kung'oa nanga mapema mwaka ujao.

0

Asilimia 80 ya maafisa wa polisi watakaoajiriwa katika awamu ijayo, watatoka katika huduma ya taifa ya vijana NYS. Hayo ni Kwa mujibu wa mwenyekiti wa tume ya taifa ya polisi Eliud Kinuthia.

Hatua hiyo ni katika juhudi za kutekeleza agizo la Rais kwamba asilimia 80 ya watakaoajiriwa katika asasi za usalama watoke katika huduma ya taifa ya vijana NYS.

Akizungumza akiwa katika eneo-bunge la Lamu Magharibi, mwenyekiti huyo, alitangaza kuwa mipango ya kuwaajiri maafisa wapya wa polisi inaendelea.

Zoezi hilo la kuajiri polisi linatarajiwa kung’oa nanga mapema mwaka ujao, ilivyotangazwa na waziri wa usalama wa taifa Prof. Kithure Kindiki mnamo mwezi Septemba.

Katika hotuba yake kwa taifa, wakati wa kikao cha pamoja cha bunge la taifa na lile la Seneti Juma lililopita, Rais William Ruto alisema asilimia 80 ya watakaojiunga na asasi za usalama, watatoka katika huduma ya taifa kwa vijana NYS.

Kulingana na Rais hatua hiyo inalenga kuongeza idadi ya vijana wanaojiunga na NYS.