Klabu ya Nottingham Forest imethibitisha kumsajili mchezaji Anthony Elanga kwa mkataba wa miaka mitano kutoka Manchester United.
Elanga mwenye umri wa miaka 21, raia wa Uswidi, ni mchezaji wa pili kusajiliwa na kocha Steve Cooper katika dirisha hili la majira ya joto baada ya Ola Aina kutua Forest kwa uhamisho huru wiki iliyopita.
“Nina furaha kubwa kuwa hapa, najivunia sio binafsi lakini pia kwa familia yangu,” Elanga aliambia tovuti ya Nottingham Forest.
“Ni hatua nyingine nzuri katika maisha yangu ya soka, natazamia sana kucheza mbele ya mashabiki wa Nottingham Forest ugani City.”
Licha ya kuvutia vlabu tofauti ikiwemo Everton, RB Leipzig na Borrusia Dortmund, Elanga alichagua Forest, hivyo ataendelea kucheza ligi ya Uingereza.
Anthony announced 🔓 pic.twitter.com/cfz96tnevg
— Nottingham Forest (@NFFC) July 25, 2023
Anthony Elanga alipokea malezi ya soka katika akademia ya Manchester United alipojiunga nao akiwa na umri wa miaka 11, na baadaye alijiunga na kikosi cha kwanza cha klabu hiyo mwishoni mwa msimu wa mwaka 2020/21 wakati wa mechi dhidi ya Leicester City, Old Trafford.
Akiwa na Manchester United Elanga amefunga mara 4 katika mechi 55 alizochezea klabu hiyo.