Mabingwa wa taifa wa mchezo wa raga ya wachezaji 15 kila upande baina ya shule za upili – All saints Embu, Vihiga na mabingwa wa taifa wa mchezo wa magongo – Musingu, wamenyakuwa ubingwa wa michezo hiyo mtawalia kwa mashindano ya Afrika Mashariki baina ya shule za upili yanayoendelea mjini Mbale nchini Uganda.
All Saints waliipiku St.Mary’s Kisubi (UG) alama tisa kwa tatu, Vihiga ikawalemea mabingwa wa taifa – Bwake alama 26 kwa nunge nayo Musingu ikailaza St.Charles magoli mawili kwa yai.
Raga ya akina dada ya wachezaji saba kila upande, pia ilishuhudia mabingwa wa taifa (St. Joseph) wakinyakua taji la Afrika Mashariki kwa kuwalemea wakenya wenzao (Kinale) alama nane kwa tano.
Kwenye nusu fainali ya mchezo wa vikapu vya wachezaji watatu kila upande, wavulana wa FSK Kamusinga waliwazaba Wakenya wenzao – Sawagongo alama 18 kwa 12 na watakabana hapo kesho katika fainali na Seroma (UG) waliowalaza Amus College (UG) alama 17 kwa 15.
Upande ule wa wachezaji watano kila upande, Laiser Hill itacheza fainali dhidi ya wenyeji – Amus College kufuatia ushindi wa vikapu 84 dhidi ya 76 vya Gasogi (RW).
Amus ilifuzu baada ya kuwazaba waganda wenzao – Buddo SS alama 62 kwa 59.
Katika nusu fainali ya voliboli ya akina dada, mabingwa wa humu nchini na pia Mabingwa watetezi wa Afrika Mashariki – Kwanzanze, waliwakwatua BCS (UG) seti tatu bila jibu za 25:13, 25:15 na 25:16 sawia na Kesogon waliowazidi nguvu St. Elizabeth (UG) seti tatu kwa nunge za 25:14, 25:20 na 25:15.
Leo vile vile kulisakatwa nusu fainali ya soka ambapo Butere walivuna ushindi wa bao moja lake Lorna Faith dhidi ya Nyakach na watachuana na St. Noa (UG) waliowazidi nguvu Amus College magoli mawili kwa moja.
Musingu walilazwa goli moja na miamba wa taji hilo St. Mary’s Kitende.