Aliyekuwa gavana wa kaunti ya Kakamega Wycliffe Oparanya na wake zake wawili, wametiwa nguvuni na maafisa wa tume ya maadili na kupambana na ufisadi EACC.
Kwa sasa Oparanya anahojiwa katika makao makuu ya EACC Jijini Nairobi, kuhusiana na tuhuma za ufisadi na uhalifu wa kiuchumi, anazodaiwa kutekeleza alipokuwa mamlakani.
Duru zinasema kuwa maafisa wa EACC wanachunguza jinsi Oparanya aliyehudumu wadhifa wa gavana wa Kakamega kati ya mwaka 2013 hadi 2022, alivyotumia shilingi bilioni 1.3.
Watatu hao kwa sasa, wanazuiliwa katika kituo cha polisi kilichoko makao makuu ya EACC, katika jumba la Integrity Jijini Nairobi.