Gavana wa Kaunti ya Kwale Fatuma Achani amezindua rasmi usambazaji wa Kompyuta 20 pamoja na vichapishaji kwa hazina za akiba na mikopo kwa wakulima kutoka wodi zote 20, ili kuboresha usimamizi wa mali na huduma zinazotolewa na hazina hizo kwa wakulima wa Kaunti hio.
Akizungumza katika makao makuu mjini Kwale, Achani amewataka wakulima zaidi ndani ya Kaunti hio kujiunga na hazina za akiba na mikopo, ili kuwawezesha kujiendeleza kimaisha kupitia kilimo biashara.
Kwa upande wake Mratibu wa miradi ya NAVCDP katika Kaunti ya Kwale Mosses Nderitu, amesema kuwa ujio wa vifaa hivyo utasaidia kuboresha utendakazi, pamoja na kuongeza usalama wa data zinazohifadhiwa na hazina hizo.