Wawakilishi wadi na ma- spika wa mabunge ya kaunti, sasa wana sababu ya kutabasamu baada ya tume ya kuwianisha mishahara na marupurupu ya watumishi wa umma-SRC kuwaongezea mishahara.
Nyongeza hiyo hii inajiri siku chache tu baada ya waakilishi wadi hao kutishia kushiriki mgomo hadi mishahara na marupurupu yao itakapoongozwa.
Katika hatua hiyo, tume ya SRC imeiongeza mshahara wa waakilishi wa Wadi kutoka shilingi 144,375 kila mwezi hadi shilingi 154,481 kuanzia mwezi Julai mwaka 2023.
Aidha, nyongeza hiyo ya mshahara itatekelezwa katika awamu mbili huku waakilishi wadi wakipokea mshahara wa jumla wa shilingi-164,588 katika kipindi cha kifedha cha mwaka-2024-25.
Viongozi wa walio wengi na walio wachache katika mabunge ya kaunti watapokea mshahara wa jumla wa shilingi-191,324 kutoka shilingi 144,375 katika kipindi kijacho cha matumuzi ya pesa na kisha mshahara wa shilingi 204,717 katika kipindi kinachofuatia.
Katika nyongeza hiyo ya SRC, Spika wa bunge la kaunti atalipwa mshahara wa shilingi 562,312 kutoka shilingi 525,525 kuanzia tarehe mosi mwezi Julai mwaka 2023.