Home Habari Kuu Afrika ina uwezo wa kuzalisha chakula cha kutosha na kujilisha, asema Rais...

Afrika ina uwezo wa kuzalisha chakula cha kutosha na kujilisha, asema Rais Ruto

0

Afrika ina uwezo wa kujilisha na nchi za bara hilo kuuza nje ya nchi mazao ya ziada.

Rais William Ruto amesema bara hilo lina uwezo mkubwa wa kufanya kilimo, uwezo anaosema linapaswa kutumia vema.

Amesema wakati umewadia kwa nchi za Afrika kufanya kazi pamoja na kutumia rasilimali zake ambazo kwa sasa zimetelekezwa.

“Tunapaswa kutumia mashamba makubwa yanayolimika kwa manufaa yetu,” alisema Rais Ruto.

Aliongeza kuwa hali nzuri ya hewa pamoja na kuajiriwa kwa vijana katika sekta hiyo kutahakikisha Afrika ina chakula cha kutosha.

Rais Ruto aliyasema hayo jana Alhamisi akiwa mjini Dar es Salaam wakati wa Kongamano la Mifumo ya Chakula barani Afrika la Mwaka 2023 lililoandaliwa na Rais Samia Suluhu.

Marais Évariste Ndayishimiye (Burundi), Hussein Mwinyi (Zanzibar) na Macky Sall (Senegal) miongoni mwa wengine walikuwapo.

Rais Ruto alionya kuwa mustakabali wa kilimo hautaafikia chochote vijana wasipohusishwa.

“Mtazamo mpya wa kilimo utawavutia vijana zaidi wanaoweza kutusaidia kuzalisha chakula kingi,” aliongeza Rais Ruto.

Rais Suluhu alisema usalama wa chakula barani Afrika umejikita kwa bara hilo kutoa usaidizi wa kifedha kwa wakulima.