Wakazi wa Gathanji, eneo bunge la Ol Joro Orok kaunti ya Nyandarua, sasa watapata huduma za serikali karibu nao, baada ya kuzinduliwa kwa ujenzi wa afisi za kaunti hiyo ndogo mpya ukianza.
Akizungumza wakati wa kuweka jiwe la msingi katika mji wa Ngano, kamishna wa kaunti ya Nyandarua Abdirisack Jaldesa, alisema wakazi wa eneo hilo kwa muda mrefu wamekumbwa na changamoto za kusafiri mwendo mrefu kutafuta huduma za serikali, lakini sasa huduma hizo zitaletwa karibu nao kufuatia ujenzi wa afisi hizo.
Kulingana na kamishna huyo wa kaunti, afisi hizo mpya pia zitapiga jeki vita dhidi ya utovu wa usalama na pombe haramu, miongoni mwa maswala mengine.
Kwa upande wake, mbunge wa eneo hilo Michael Muchira, alidokeza kuwa serikali ya taifa kupitia wizara ya usalama wa taifa na hazina ya ustawi wa maeneo bunge NGCDF, imetenga shilingi milioni 20 na shilingi milioni 5 mtawalia kwa ujenzi wa afisi hiyo.
Mbunge huyo alisema mradi huo utabuni nafasi za ajira kwa vijana na utaimarisha biashara katika eneo hilo la Ngano.
Utakapokamilika, mradi huo unatarajiwa kuwiainisha michakato ya utawala na kushughulikia mahitaji ya idadi ya watu inayozidi kuongezeka.