Afisa mmoja wa zamani wa vikosi vya ulinzi vya Kenya (KDF), siku ya Jumatatu alifikishwa katika mahakama ya milimani akikabiliwa na mashtaka matano ya uchapishaji wa habari za uongo na dhulma za mtandaoni.
Franklin Opiyo Ogonji alifikishwa mahakamani kwa kuchapisha habari za uongo kumhusu mkuu wa vikosi vya ulinzi Jenerali Francis Ogolla, kwenye ukurasa wake wa Facebook.
Kulingana na upande wa mashtaka,afisa huyo wa zamani wa KDF, alimnyanyasa mkuu wa majeshi ya Kenya generali Ogolla.
Makosa hayo yanadaiwa kutendwa tarehe tofauti kati ya tarehe tisa mwezi Disemba mwaka 2022 na tarehe 24 mwezi Julai mwaka huu, kwa lengo la kuibua taharuki na ghasia miongoni mwa wananchi.
Mshtakiwa ambaye alikamatwa tarehe 25 mwezi huu, alikanusha mashtaka na akamuomba hakimu BenMark Enkhubi amuachilie kwa thamana isiyokuwa na malipo akisema anapata riziki yake kupitia kwa michezo ya bahati na sibu.
Opiyo aliachiliwa kwa thamana ya shillingi elfu mia moja na mdhamini wa kiasi kama hicho au thamana ya shillingi 50,000 pesa taslimu.
Kesi hiyo itatajwa tarehe 15 mwezi Septemba mwaka huu.