Home Habari Kuu Afisa wa REREC ashtakiwa kwa kughushi cheti cha masomo

Afisa wa REREC ashtakiwa kwa kughushi cheti cha masomo

0

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC jana Jumatatu ilimkamata Eunice Ngima Gachugi na kumfikisha katika mahakama ya kupambana na ufisadi.

Gachugi ni afisa wa usimamizi wa mtungo wa usambazaji katika shirika la umeme na nishati mbadala la Rural Electrification and Renewable Energy Corporation, REREC.

Afisa huyo anadaiwa kughushi vyeti vya masomo ili kupata ajira katika shirika hilo.

Alipofikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Thomas Nzyoki, Gachugi alikanusha kuwa alighushi cheti cha stashahada katika masomo ya taarifa ya biashara na teknolojia. Alidai cheti hicho ni halali na alikipata kutoka Chuo Kikuu cha Kenya Methodist.

Anakabiliwa na mashtaka matano ikiwa ni pamoja na kughushi cheti cha stashahada, kutoa taarifa za uongo kwa mtu aliyeajiriwa katika utumishi wa umma na kulipwa mshahara wa shilingi 293,457.07 kutoka kwa fedha za umma kinyume cha sheria.

Anadaiwa kupokea fedha hizo kwa kipindi cha miezi mitatu kabla ya kujiuzulu wakati EACC ilipoanza kufanya uchunguzi.

Mshtakiwa aliachiliwa kwa dhamana ya shilingi 200,000 pesa taslimu au dhamana ya shilingi 500,000.

Kesi hiyo itatajwa Machi 25, 2024.

Website | + posts