Maafisa wa polisi wanachunguza kisa ambapo afisa wa polisi alimpiga risasi afisa mwenzake na kumuua siku ya Jumanne asubuhi.
Kamanda wa polisi kaunti ya Nakuru Samuel Ndanyi, alisema tukio hilo lilitokea katika makao makuu ya maafisa wa polisi wa kitengo cha mbwa eneo la Rift Valley, Nakuru mashariki.
Kulingana na kamanda huyo wa polisi, mshukiwa ambaye ni wa cheo cha konstabo Jackson Konga, alimpiga risasi sajenti Christopher Kimeli katika mazingira tatanishi.
Kamanda huyo alisema mshukiwa kwa sasa anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Central Jijini Nakuru.
Tukio hilo linajiri huku wasiwasi ukiibuka kuhusu afya ya kiakili ya maafisa wa polisi na wakenya kwa jumla.