Rais wa Tanzania Samia Suluhu anasema watu 57 wamethibitishwa kufariki kufikia sasa kutokana na mafuriko nchini humo.
Wengine 85 wanaendelea kupata matibabu katika hospitali mbalimbali.
“Mpaka sasa tumewapoteza ndugu zetu 57 katika maafa haya huku 85 wakiendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, Hospitali ya Wilaya ya Hanang na Kituo cha Afya Gendabi,” amesema Rais Suluhu wakati akizungumzia mafuriko yaliyoikumba nchi hiyo.
Kutokana na hali hiyo, Rais Suluhu amemuelekeza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kupitia Idara ya Uratibu wa Shughuli za Maafa na Serikali ya Mkoa kuhakikisha serikali inagharimia mazishi ya waliofariki, igharimie matibabu ya majeruhi wote na iwape makazi ya muda wote waliopoteza makazi yao.
Vitengo na taasisi zetu zote za zerikali zinazohusiana na maafa pia zimeagizwa kuwepo eneo la tukio na kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha hali inarejea kawaida na kufanya tathmini ya maafa hayo.
“Wakati serikali ikiendelea na juhudi hizi, tuendelee kuwaweka katika dua na maombi wote walioathirika na maafa haya,” aliongeza Rais Suluhu.