Home Burudani 50 Cent aumiza mwanamke kwa kipaaza sauti

50 Cent aumiza mwanamke kwa kipaaza sauti

0

Mwanamuziki wa Marekani Curtis Jackson maarufu kama 50 Cent alirusha kipaaza sauti kutoka jukwaani kwenye tamasha ya hivi maajuzi ambacho kilimgonga na kumuumiza mwanamke aliyekuwa kwenye tamasha.

Video ya kisa hicho cha Jumatano katika ukumbi wa Crypto huko Los Angeles imetolewa na inamwonyesha mwanamuziki huyo akitupa vipaaza sauti viwili kutoka jukwaani na mara ya pili alitumia nguvu nyingi.

Inasemekana wasimamizi wa jukwaa walimpa kipaaza sauti ambacho hakikuwa kikifanya kazi akakidondosha karibu na jukwaa, wakampa cha pili nacho kikawa hakitoi sauti na kwa ghadhabu akakitupa.

Alipatiwa cha tatu kikawa kinafanya kazi na akaendelea kutumbuiza.

Aliyeumizwa na kipaaza sauti hicho ni mtangazaji wa kituo cha redio cha Power 106 Bryhana Monegain, ambaye alikuwa amesimama katika upande ambao wasimamizi na waandalizi wa tamasha walikuwa.

Picha zake baada ya tukio zinaonyesha kwamba aliumia kwenye kipaji cha uso kiasi cha kuvuja damu.

Wakili wa 50 Cent, Scott Leemon, alitetea mteja wake akisema hakufanya vile kimakusudi.

50 Cent anaendeleza ziara yake ya kikazi kwa jina “The Final Lap Tour” ya kusherehekea miaka 20 tangu atoe albamu yake ya kwanza iitwayo, “Get Rich or Die Tryin”.

Julai mwaka huu, Cardi B naye alihusika kwenye kisa sawia katika eneo la burudani la Drai’s Beachclub huko Las Vegas. Alimlenga shabiki aliyemmiminia kinywaji kwa kipaaza sauti.