Utimizaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) unaathiriwa na ukosefu wa fedha na kuna haja ya kutafuta fedha zaidi kando na fedha za kawaida zinazotengwa na serikali.
Hii ni kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Kongamano la SDG Kenya Florence Syevuo.
Akizungumza wakati wa kongamano la washikadau lililoandaliwa ili kutathmini mchakato wa Malengo ya Maendeleo Endelevu baada ya mwaka wa 2015, Syevuo alisema kulikuwa na hatua mseto iliyopigwa katika utimizaji wa malengo hayo huku baadhi yakitimizwa wakati mengine yakisalia nyuma.
Alitaja lengo namba 13 kuhusiana na mabadiliko ya tabia nchi akisema hatua inayopaswa kupongezwa ilipigwa kutokana na upanzi wa miche ingawa mengi zaidi yanapaswa kufanywa.
Kuhusiana na lengo namba 1, mkurugenzi huyo alisema kulikuwa na upungufu wa vyanzo vya kupata riziki kutokana na athari za janga la virusi vya korona na vita nchini Ukraine vilivyosababisha ukosefu wa ajira.
Lengo namba 2 linalohusu usalama wa chakula linakabiliwa na changamoto kwani kumekuwa na usambazaji usiotosheleza na kusababisha kupanda kwa bei za chakula.
Syevuo alisema utimizaji wa lengo namba tatu ulikuwa wa wastani kwani kulikuwa na vituo zaidi vya afya vilivyojengwa na serikali za kaunti. Hata hivyo, alisema bado kulikuwa na changamoto za upatikanaji wa dawa za kutosha kwenye vituo hivyo na madaktari wa kutosha kuwahudumia wagonjwa.
Julius Chokera ni afisa wa maendeleo anayefanya kazi na Ofisi ya Uratibu wa Ukazi ya Umoja wa Mataifa. Alisema kuna haja kuangazia upya Malengo ya Maendeleo Endelevu kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali.
Kulingana naye, pia kuna haja ya kuangazia malengo yanayohusiana na upatikanaji wa nishati kijani ili kuchochea utengenezaji bidhaa na kubuni nafasi za ajira.
Imelda Achieng ni Afisa Mkuu Mtendaji wa kundi la bunge la Kenya linaloangazia Malengo ya Maendeleo Endelevu na Biashara. Alisema kuna wabunge 30 ambao wameahidi kupigia debe kwa hiari utimizaji wa malengo hayo.
Alisema kuna changamoto katika utimizaji wa malengo yanayofungamana na maono ya mwaka 2030 kwani kuna rasilimali chache na matumizi ya kawaida ya seriikali yapo juu mno.
Kongamano la Malengo ya Maendeleo Endelevu lilileta pamoja mashirika ya kijamii, wawakilishi kutoka Umoja wa Mataifa, serikali ya kitaifa na Baraza la Magavana miongoni mwa washikadau wengine.