Home Kaunti Jamii za wachache Narok zalalamikia kubaguliwa katika ugavi wa msaada wa masomo

Jamii za wachache Narok zalalamikia kubaguliwa katika ugavi wa msaada wa masomo

Jamii za wachache katika kaunti ya Narok zimelalamikia kile zinazotaja kuwa kubaguliwa katika usambazaji wa msaada wa masomo wa shilingi milioni 350 uliotolewa na Gavana Patrick Ntutu.

Wakiongozwa na Mercy Otuni watu wa jamii hizo wananyosha kidole cha lawama kwa waliopatiwa jukumu la kugawa msaada huo wa masomo kwa kudhihirisha upendeleo.

Otuni anasema kwamba wakazi wa wadi ya Narok Mjini bado hawajafaidika na msaada huo wa masomo na kwamba wanafunzi werevu wanaotoka jamii maskini bado hawajakwenda shule.

Kulingana naye mji wa Narok una watu wa jamii mbali mbali za Kenya na wanaomba Gavana aingilie kati awasaidie.

Kiongozi wa vijana katika chama cha watu wa jamii za wachache katika kaunti ya Narok Joab Otipi anaelezea kwamba tayari wametoa orodha ya majina ya wanaohitaji msaada wa masomo kwa afisi ya Gavana lakini bado hawajapata jibu lolote.

Otipi anasema serikali ya kaunti ya Narok ilitoa shilingi milioni 12 za msaada wa masomo kwa wadi ya Narok Mjini na anadai pesa hizo ziliishia mikononi mwa mwakilishi wadi na waziri wa kaunti.

Mwenyekiti wa chama hicho Maurice Owinga ametoa makataa ya siku saba kwa gavana Ntutu kusuluhisha suala hilo la sivyo watafanya maandamano ya amani hadi afisini kwake.

Website | + posts
Stanley Mbugua
+ posts