Home Habari Kuu Ruto: Serikali inatekeleza mipango itakayoboresha maisha ya Wakenya

Ruto: Serikali inatekeleza mipango itakayoboresha maisha ya Wakenya

0

Serikali inaifanyia mabadiliko Hazina ya Bima ya Afya ya Kitaifa, NHIF ili kuharakisha upatikanaji wa afya kwa wote. 

Rais William Ruto amesema serikali inanuia kutoa bima ya afya ya umma yenye bei nafuu na inayowajumuisha watu wote.

Alisema Wakenya wengi wasiokuwa na ajira rasmi sasa watatarajiwa kulipa ada ya shilingi 300 kwa NHIF zikiwa zimepunguzwa kutoka shilingi 500.

Aidha, alisema serikali itawalipia wale wasiojiweza ada hiyo.

“Hakuna Mkenya atakayelazimika kuuza mali yake ili kupata huduma za afya,” alisema Rais.

Aliyazugumza hayo leo Ijumaa alipotoa zawadi za Ksrimasi kwa wakazi wa eneo bunge la Turbo na maeneo jirani nyumbani kwake huko Sugoi, kaunti ya Uasin Gishu.

Alikuwa ameandamana na mkewe Rachel Ruto na Magavana Johnson Sakaja wa Nairobi na Jonathan Bii wa kaunti ya Uasin Gishu miongoni mwa viongozi wengine.

 

Kiongozi wa nchi alisema serikali itaendelea kutekeleza mipango itakayoongeza fursa za ajira akitoa mfano wa mpango wa nyumba za bei nafuu na Hazina ya Hustler.

“Hadi kufikia sasa, watu zaidi ya 120,000 wameajiriwa katika mpango wa nyumba za bei nafuu,” alisema Rais Ruto.

Alitoa wito kwa Wakenya kutumia Hazina ya Hustler kuanza na kuunga mkono shughuli za kuwaingizia mapato.

Aliongeza kuwa serikali yake itaendelea kutekeleza mabadiliko katika sekta ya kilimo, akisema mabadiliko yaliyotekelezwa katika sekta hiyo hadi kufikia sasa yamesababisha ongezeko la asilimia 40 la uzalishaji wa chakula mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana.

“Nawataka kuwashukuru wakulima kwa kutumia mabadiliko hayo kujinufaisha ikiwa ni pamoja na mbolea ya bei nafuu iliyopunguzwa bei kutoka shilingi 7,000 hadi 2,500. Tutaendelea kuifanyia sekta hiyo mabadiliko zaidi ili kuboresha uzalishaji,” alisema Rais.

Martin Mwanje & PCS
+ posts